Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kigwangalla amesema kuwa Serikali kupitia Halmashauri zilizo katika maeneo ya migodi imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa ya Kifua kikuu na Silicosis kwa kutoa Elimu kwa wachimbaji wa madini.
Ameyasema hayo mapema hii leo bungeni Mjini Dodoma wakati wa maswali na majibu, amesema kuwa kupitia ufadhili wa mfuko wa Dunia wa kupambana na Magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria Global Fund to Fight AIDS, nchi kumi za Jumuiya wanachama wa SADC ikiwemo Tanzania ziko katika utekelezaji huo.
“Tanzania inafahamu changamoto ya uwepo wa magonjwa haya ya kifua kikuu na Silicosis katika maeneo ya wachimbaji, kwa upande wa Kifua kikuu tatizo hili ni kubwa lakini hakukuwepo na ripoti za wagonjwa wachache wa Silicosis katika hospitali za Serikali ikiwemo Kibong’oto”,Amesema Kigwangalla.
Aidha katika mpango huo kuna kitengo kitakacho shughulika na sera za udhibiti wa vumbi katika maeneo ya wachimbaji ambayo itawabana wachimbaji kudhibiti vumbi wakati wa shughuli za uchimbaji.
Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali itaongeza wigo wa huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo yaliyoathirika ikiwemo Mkoa wa Geita ili vituo viwe na uwezo wa kuchunguza na kutibu magonjwa hayo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya katika kuhudumia wagonjwa katika maeneo ya migodi.