Serikali imepiga marufuku shule binafsi na za umma kuwasimamisha masomo au kuwafukuza shule wanafunzi kwa sababu za kutokamilisha ada/karo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amesema kuwa kuanzia kesho hataki kusikia kuna shule ambayo imeenda kinyume na maagizo hayo.
“Nina ujumbe ambao nimetumiwa na wazazi kuhusu shule ambazo zimewarudisha watoto nyumbani kwa kukosa ada na malipo mengine ya kiholela kama vile kulazimishwa kununua sare za shule shuleni, madaftari ya ganda gumu, na rim paper (karatasi),” amesema Waitara.
Kutokana na ujumbe huo, amewataka Maafisa elimu, Wakurugenzi na Makatibu Tarafa kufika kesho katika shule hizo zilizotajwa kuwa zimewarudisha nyumbani wanafunzi na kumpa mrejesho haraka.
Kutokana na hatua hiyo, Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa anafikiria suala la kurejesha mjadala wa malipo ya ada elekezi kwa ajili ya shule binafsi.
“Hili halivumiliki hata kidogo, wakibainika wanaofanya hivyo tutawachukulia hatua kwa sababu wao hawalipi kodi na wanatoa huduma. Na nawakumbusha tu kuwa elimu inasimamiwa na Serikali,” alisema Waitara.
Alisema zipo shule ambazo zinaweka kiwango kikubwa cha ada cha kati ya shilingi milioni 1.5 hadi Milioni 6 na bado zinaeleza kuwa zinatoa huduma na sio biashara.
Ameeleza kuwa shule hizo huweza kumsimamisha mwanafunzi aliyekuwa amelipa ada kwa miaka mitatu mfululizo lakini amekosa kulipa ada hata ndani ya kipindi cha wiki moja na haruhusiwi kufika shuleni bila kuwa na stakabadhi ya kukamilisha ada.