Waziri Mkuu wa mpito wa Haiti Claude Joseph, ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu kutokea kwa mauaji ya rais Jovenel Moise, amekubali kujiuzulu ili kupisha nafasi ya kuundwa serikali mpya itakayozijumuisha pande zote, na itakayoongozwa na mtu ambaye Moise alimteuwa siku kadhaa kabla ya kuuliwa.
Serikali hiyo mpya, ambayo inatarajiwa kuchukua usukani leo, haitakuwa na rais, na itapewa jukumu la kuandaa uchaguzi mpya haraka iwezekenavyo.
Moise alimteuwa Ariel Henry kuchukua nafasi ya Joseph kama waziri mkuu siku chache tu kabla ya rais huyo wa Haiti kupigwa risasi nyumbani kwake mjini Port-au-prince usiku wa Julai 7.
Henry atachukua wadhifa huo Kufuatia mauaji ya Joseph alitangaza sheria ya kijeshi na kusema yuko usukani, hatua iliyozusha msuguano wa madaraka katika taifa hilo maskini la Caribbean.
Tangazo hilo la jana limeongeza matumaini ya kumaliza sintofahamu iliyokuwepo, baada ya Marekani, ambayo ina ushawishi mkubwa nchini Haiti, kuungana na madola mengine katika kumtaka Joseph kuwachia madaraka.