Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali kukabiliana na changamoto ya afya ya akili ambayo inawakumba Watanzania wengi kwasasa hususan kwenye maeneo yakazi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako ameyasema hayo wakati akiwahutubia Wanamichezo walioshiriki Bonanza la Waajiri lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania –
ATE, katika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali itaendelea kuweka mipango ya kisera na kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma kwa Wananchi pamoja na kujenga vituo vya afya nchi nzima na kuongeza wataalamu.
“Licha ya uwepo wa changamoto ya afya ya
akili, Wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi wamekuwa wakikabiliana na tishio la magonjwa yasiyoambukiza kama vile, Saratani,
magonjwa ya moyo, Kisukari na Magonjwa
haya kwa kiasi kikubwa yamekuwa yanasababishwa na mtindo wa maisha sambamba na kutokuwa na tabia ya kufanya mazoezi,” amesema Prof. Ndalichako.
Naye Katibu Mkuu katika ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja pamoja na kuwapongeza ATE, amesema Bonanza hilo ni changamoto kwa Wizara yenye dhamana ya masuala ya Ajira na
Vijana ambapo ndio walipaswa kuandaa.