Serikali kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi, maji na maslahi ya watumishi inayoukabili mkoa wa Kilimanjaro ambapo wananchi wameahidiwa kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto hizo.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Samia Suluhu Hassan leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 wakati akizindua barabara ya Sanya Juu – Elerai iyojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 32.2 na inagharimu kiasi cha Sh62.7 bilioni.
“Tunapita kuangalia yaliyotendeka na kuona changamoto zilizopo na hapa naona mabango mengi, kuna migogoro ya ardhi na maslahi ya wafanyakazi naomba tuyakusanye halafu tutakwenda kuyafanyia kazi”.
“Changamoto hizi tutakwenda kuzifanyia kazi na ahadi yetu CCM ni kuangalia kero za wananchi na kuzifanyia kazi,” amesema Rais Samia
“Najua hapa Kilimanjaro kuna changamoto ya maji na migogoro ya ardhi ambayo ndio kubwa zaidi n azote hizi nimeziona kwenye mabango hivyo, nitazichukua kwenda kuzichambua na kuzifanyia kazi.”
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Rogatus Mativila amesema ujenzi huo ulianza mwaka 2019.