Waziri Mkuu wa Mali, Soumeylou Boubeye Maiga na Baraza lote la Mawazili wamejiuzulu kutokana na shinikizo la umma kwa kushindwa kutuliza hali ya vurugu ndani ya nchi hiyo.
Jana, Bunge lilikuwa linajiandaa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wakidai kuwa ameshindwa kurejesha hali ya utulivu na kuwalinda raia dhidi ya makundi ya kigaidi na yale ya kikabila.
Mwezi uliopita, mamia ya wafugaji waliuawa nchini humo na watu wanaosadikika kuwa ni wa kabila hasimu kwao.
Rais wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keita amesema kupitia taarifa yake kwa umma kuwa amekubali uamuzi wa Waziri Mkuu pamoja na mawaziri wake wote na kwamba anatarajia kuunda Baraza jipya la mawaziri hivi karibuni.
“Tutamtaja Waziri Mkuu hivi karibuni na Baraza jipya la Mawaziri litatangazwa baada ya kufanya mashauriano na viongozi wengine wa kisiasa,” alisema Rais Keita.
Mali imekuwa kwenye janga la kupambana na kundi lenye uhusiano na Al-Qaeda tangu mwaka 2015, licha ya jitihada za kijeshi za nchi hiyo, kundi hilo limeendelea kufanikiwa kujitanua na hata kuzishika sehemu zenye idadi kubwa ya watu.
Aidha, mauaji yanayotokana na vita za kikabila yameendelea kuongozeka, ambapo miezi kadhaa iliyopita watu wa wanaoaminika kuwa ni wa kabila la Dogon lilivamia na kuua watu 160 wa kabila la Fulani, hali iliyoongeza taharuki na kusababisha watu kuanza kuishinikiza Serikali kujiwajibisha.