Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi na kiongozi wa upinzani nchini humo, Ossufo Momade wamesaini makubaliano ya kihistoria yanayolenga kumaliza rasmi miongo mingi ya uhasama.
Makubaliano hayo ya kihistoria yamesainiwa katika mbuga ya kitaifa ya Gorongosa iliyopo jimbo la kati nchini Msumbiji.
Aidha, mkataba huo uliosainiwa jana Alhamisi, unamaliza mchakato mrefu wa mazungumzo ya amani ulioanzishwa na kiongozi wa kihistoria wa chama cha upinzani cha Renamo, Afonso Dhlakama aliyefariki mwezi Mei mwaka uliopita.
Rais Nyusi amesema kuwa makubaliano hayo yanafungua enzi mpya ya historia ya Msumbiji, ambapo hakuna raia wa Msumbiji atakayehitajika kutumia silaha kusuluhisha mzozo.
“Tunajua migogoro ya vita imesababisha vifo vya ndugu zetu wengi na uharibifu wa mali binafsi. Kama Wanamsumbiji tumeweka kumbukumbu za uchungu kuhusu kipindi kigumu cha historia yetu kama funzo la kuzuia isijirudie.” amesema Rais Nyusi
Kwa upande wake, kiongozi mpya wa chama cha Renamo aliyechukua usukani kutoka kwa Dhlakama, Ossufo Momade amesema kuwa wanataka kuwahakikishia watu na dunia kwa ujumla kwamba wameizika dhana ya kutumia vita kama njia ya kusuluhisha tofauti zao.
“Hii ni tarehe ya kihistoria kwasababu baada ya miaka mingi ya migogoro sisi kama ndugu, tumejitolea kuweka amani inayotakiwa na wote kwa manufaa ya nchi.” amesema Momade
-
Boko Haram wafanya shambulio mazishini, 65 wauawa vibaya
-
Zimbabwe yakerwa na vikwazo vya Marekani dhidi balozi wake nchini Tanzania
Nchi ya Msumbiji ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wareno mnamo mwaka 1975, Renamo iliongoza vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 16 dhidi ya serikali ya chama cha Frelimo, ambapo vita hivyo vilisababisha vifo vya watu milioni moja na vilimalizika mwaka 1992.