Serikali ya Nigeria imetangaza ilani ya marufuku ya kutoka nje katika majimbo ya Rivers na Delta kufuatia ongezeko la ghasia zinazoendelea dhidi ya kikosi maalum cha kupambana na wizi (SARS), kilichoundwa na polisi.

Gavana wa jimbo la Rivers, Nyesom Wike, alitangaza ilani ya marufuku ya kutoka nje kwa muda wa masaa 24 kutokana na ghasia kuzidi wakati akithibitisha kuuawa kwa watu 8, wakiwemo maafisa 3 wa polisi kwenye maandamano ya jana.

“Majengo ya polisi ya mkoa wa Oyigbo na mahakama yalishambuliwa na kuchomwa moto na watu wasiojulikana, mali nyingi pia ziliharibiwa kwenye ghasia hizo zinazoendelea katika mkoa wa Ikokwu, hivyo basi, ilani ya marufuku ya kutoka nje kwa masaa 24 imetangazwa katika jimbo hilo ili kuzuia vurugu,” amesema Wike.

Gavana wa jimbo la Delta, Ifeanyi Okowa pia amesema kuwa kuanzia saa 12 kamili jioni, hakutoruhusiwa mtu kutoka nje kwa muda wa masaa 48 isipokuwa wahusika wa kutoa huduma za kimsingi pekee ndio watakaoruhusiwa.

Okowa pia amearifu kufungwa kwa shule za msingi na za sekondari hadi tarehe 2 Novemba kutokana na maandamano ya ghasia.

Apasuka korodani akiwa uwanjani
Akumu aibuka tena Young Africans