Serikali ya Tanzania imeishukuru China kwa kuipatia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kompyuta mpakato 20 zitakazowasaidia katika shughuli za ufundishaji na kuboresha utendaji kazi kwa watumishi wa chuo hicho.
Akipokea kompyuta hizo kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Wang Ke, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) amemshukuru Balozi huyo kwa mchango wao katika kuboresha Chuo hicho kwa maendeleo ya taifa.
Mkuchika amepongeza ushirikiano ambao China imekuwa nao kwa Chuo cha Utumishi wa Umma katika masuala mbalimbali ya kuboresha utendaji ikiwa ni pamoja na watumishi wa chuo hicho kushiriki semina mbalimbali nchini China ambazo zinawasaidia kuongeza ujuzi.
Aidha, Mkuchika amemuomba Balozi huyo kusaidia katika ujenzi wa tawi jipya la chuo hicho linalotarajiwa kujengwa jijini Dodoma baada ya Serikali kuhamishia shughuli zake Makao Makuu ya nchi Dodoma na kuongeza kuwa ujenzi wa chuo hicho utatoa fursa kwa watumishi waliohamia Dodoma na mikoa jirani kuongeza ujuzi katika Chuo hicho.
Kwa upande wake Balozi Wang Ke amefafanua kuwa, anatamani kukiona Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kikitoa elimu bora zaidi na kikizalisha watumishi wa umma bora nchini.
Hata hivyo, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maafisa kutoka ubalozi wa China nchini Tanzania wakiongozwa na Balozi Wang Ke, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.