Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba ameziagiza halmashauri zote nchini kutenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya vijana kuzalisha mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Ametoa agizo hilo leo februari 28, 2020 mjini Njombe wakati alipofungua kongamano la vijana wa mikoa ya Njombe,Ruvuma na Iringa kujadili fursa zilizopo katika sekta ya kilimo nchini.
Mgumba amesema kumekuwepo na malalamiko ya vijana kukosa ardhi kutokana na halmashauri kuwa na mashamba pori mengi yasiyopimwa na kulimwa.
“Halmasahauri zote zihakiki mashamba pori yote au yaliyochukuliwa mikopo na hayalimwi yapimwe na kugawiwa kwa vijana walio tayari kufanya kazi za kilimo nchini” alisema Naibu Waziri Mgumba.
Ili kufanikisha hilo Mgumba amewataka vijana kujisajili kwenye daftari la wakulima linaroratibiwa na wizara yake ili serikali iwatambue na kujua changamoto zao na kisha kuwaonyesha fursa za ajira kwenye kilimo.
Amesisitiza halmashauri nchini kutoa fedha za mikopo kwa vijana bila urasimu ili vijana wanufaike na kuanzisha kazi za uzalishaji mazao ya kilimo na mifugo.
Mgumba amewafahamisha kuwa serikali imeelekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuendelea kutoa mikopo kwa vijana ili wapate mitaji.
“Wapo vijana wengi wasomi wameamua kujiajili katika kilimo ili kufikia malengo ya kuongeza ajira ikiwa ni malengo ya Serikali ya awamu ya tano kukuza sekta ya kilimo” amesema Mgumba.
Na kuongeza “Tanzania ina eneo la hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo hivyo vijana wajitokeze kutumia fursa hiyo kuanzisha kazi za kuzalisha mazao ya kilimo”.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri, ameziagiza halmashauri zote za mkoa wa Njombe kuandaa katiba kwa ajili vijana kushiriki shughuli za kilimo.