Halmashauri zote nchini zimeagizwa kutumia mfumo wa kieletroniki katika malipo yote na makusanyo ya mapato yanayofanyika ili kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa fedha na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha zinazokusanywa.

Agizo hilo la Serikali limetolewa leo bungeni mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akitoa hoja ya kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge la 11.

Waziri Mkuu alisema kuwa kuanzia Julai mosi mwa huu, tarehe ambayo itakuwa mwanzo wa mwaka mpya wa fedha (2016,17), kila halmashauri ihakikishe inatumia mfumo wa kieletroniki katika kulipa, kuweka na kukusanya mapato yote ya Halmashauri hata kama ni kwa kutumia mawakala. Alisema kuwa lengo ni kupunguza kwa kiasi kikubwa na hatimaye kuondoa kabisa utaratibu wa kufanya malipo kwa kutumia fedha taslimu.

Waziri Mkuu pia aliziagiza Halmashauri kuwatumia zaidi mawakala katika kukusanya mapato ili kutoa nafasi kwa watumishi wa halmashauri hizo kuendelea na majukumu mengine.

Hata hivyo, alizitaka Halmashauri hizo kuhakikisha mapato yote yanawekwa kwenye akaunti ya halmashauri haraka na kwamba mawakala wanapaswa kulipwa baada ya kuweka kwenye akaunti hizo fedha walizokusanya.

Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya Serikali pamoja na michango ya wananchi. Alisema uzoefu unaonesha kuwa mamlaka hizo zina tatizo la kukaa na fedha kwa muda mrefu kabla ya kuzielekeza kwenye matumizi yaliyokusudiwa.

“Kuchelewesha kutoa fedha zilizotengwa kwa shughuli zilizopangwa ni kuchelewesha kufikisha huduma muhimu kwa wananchi. Napenda kuhimiza uzingatiaji wa utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya fedha za Serikali katika ngazi zote ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya umma,” alisema.

Mkutano huo wa tatu wa Bunge ulioanza Aprili 19, 2016 ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 6, mwaka huu litakapokutana tena mjini Dodoma.

Video: Waislam kuadhimisha siku ya 'QUDS' leo
Lebo Za Kusimamia Kazi za wasanii Zinakuza Mziki wa Bongo?