Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa fedha za kugharamia mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) ili ukamilike kwa wakati.

Ameyasema hayo baada ya kukagua mwenendo wa mradi huo, unaotarajiwa kukamilika June 2022 ambapo ameahidi kuwa Serikali itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.

Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona kazi nzuri yenye viwango na ubora wa hali ya juu inayofanywa na Kampuni ya Arab Contractors kwa pamoja na ile ya Elsewedy  Electric zote kutoka nchini Misri chini ya usimamizi wa TANESCO, TANROADS na Wizara ya Nishati.

Majaliwa amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha Watanzania kupata umeme mwingi na wa gharama nafuu ambao utasambazwa nchini kote na ziada kuuzwa nje ya nchi ili kulipatia Taifa fedha za kigeni.

Waziri Mkuu amesema bwawa hilo linatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 ambazo zikijumlishwa na megawati 1,500 zinazozalishwa na vyanzo mbalimbali nchini hivi sasa zitaifanya Tanzania kuwa na umeme utakaotosheleza mahitaji yake na ziada kuuzwa kwa majirani.

“Lengo la kuanzisha mradi huu ni moja ya juhudi za Serikali za kupunguza gharama za umeme kwa wananchi kwa sababu uzalishaji wake ni wa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine. Uniti moja ya umeme unaozalishwa kwa kutumia maji inagharimu shilingi 36 hadi shilingi 50 huku umeme unaotumia vyanzo vya mafuta uniti moja inazalishwa kwa gharama ya shilingi 440 hadi shilingi 600,” amesema Majaliwa.

Gharama/Bei za umeme kwa unit kutokana na vyanzo vingine ni: upepo shilingi 103.5, jua shilingi 103.5, Makaa ya Mawe shilingi 114, Jotoardhi shilingi 118, Nyuklia shilingi 65, Gesi shilingi 147.

Faida za vitunguu swaumu kwa wanaume
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 11, 2021