Serikali imeahidi kuendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa kushirikiana na vyombo vya habari ili kwa pamoja kuweza kuhamasisha, kuunda na kujenga nchi ya viwanda katika kuunga mkono azma ya Rais Mhe. John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Mchezo, Nape Moses Nnauye alipokutana na wamiliki na watendaji waandamizi wa vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Nnauye amesema kuwa Serikali na vyombo vya habari wakishirikiana na kuwa na lengo moja wataweza kuileta Tanzania pamoja na kuiweka katika mwelekeo ulio sahihi.
“Tukiamua leo kila chombo cha habari kikawa na dawati maalumu linalozungumzia Tanzania ya viwanda kama ilivyo kwa madawati mengine ndani ya vyombo vyetu vya habari, na Serikali ikaendelea kutoa hamasa za uanzilishwaji wa viwanda ambavyo vitasukumwa na dawati hilo maalumu la viwanda, tutaweza kutimiza ndoto yetu ya Tanzania ya Viwanda” amesema Nnauye
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Francis Nanayi kutoka Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi amesema kuwa ili vyombo vya habari viweze kutangaza habari vinahitaji kupata ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini kuonyesha mikakati na malengo ya serikali kuwezesha vyombo vya habari kujenga Tanzania ya viwanda na kuwapa fursa wananchi kupata taarifa sahihi za nchi.
Naye Mtendaji kutoka Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabe Masasi amesema kuwa Mapinduzi ya viwanda yanaweza kufanyika kama vyombo vya habari vitatoa taarifa sahihi za upatikanaji wa malighafi za uwekezaji kulingana na mahitaji yaliyopo katika maeneo husika na kuwekeza katika viwanda vidogovidogo vitakavyozalisha viwanda vikubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari Dkt. Hassani Abbas amesema kuwa atahakikisha maafisa habari wa Serikali hususani maafisa wanaohusika na Sekta ya viwanda wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya habari ili kuweza kuelimisha umma namna Tanzania ya Viwanda inavyojengwa.