Serikali imesema kuwa itaendelea kuvilinda Vyombo vya Habari vilivyowekeza nchini zikiwemo Radio na Televisheni kwa kuwa mchango wao katika jamii ni mkubwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Nape Nnauye katika ziara yake kwa Vyombo vya Habari vya E-fm, TV1 na Times Fm, leo Jijini Dar es Salaam.

“Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mikubwa ya kuwa karibu na Vyombo vya Habari nchini, kupitia Wizara yangu tunautambua uwekezaji huu mkubwa mlioweka katika Teknolojia na tunatambua gharama kubwa iliyotumika, hivyo Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ili uwekezaji huu usonge mbele,”amesema Nape.

Aidha  Nape amesema kuwa uwekezaji uliofanyika kupitia vituo hivyo vya Mawasiliano sio rahisi na ni vyema kuheshimu uwekezaji huo kwa kila namna kwani umeonyesha njia na ana imani kuwa wengi wataiga mfano huo wa uwekezaji.

Nape ametumia fursa hiyo pia kuvishukuru Vyombo vya Habari nchini kwa kuanzisha vipindi ambavyo vinabeba ajenda ya viwanda na kutoa wito kwa vyombo vingi zaidi kubuni vipindi kama hivyo ili watanzania wengi wapate fursa zaidi ya kuelewa dhana nzima ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Vile vile, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kupitia Sheria na Kanuni zilizopo na kuzifanyia marekebisho ili kutengeneza daraja zuri kati ya Serikali na wadau wa Habari ikiwa ni pamoja na kuboresha mahusiano katika kazi kwani Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na vyombo hivyo.

Hata hivyo, ziara hiyo ni muendelezo wa ziara za kikazi za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye katika Vyombo vya Habari nchini kwa lengo la kujifunza na kuimarisha yaliyopo baina ya Serikali na Vyombo vya Habari nchini.

Video: Mafuriko yalikumba Jiji la Dar
Video: Vikundi vya Vicoba Dar vyatakiwa kujisajili