Naibu Waziri wa Afya, Godwin Mollel, amesema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya upandikizaji wa viungo nchini, Serikali imeandaa Muswada wa kutunga sheria itakayoongoza taratibu za uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa viungo.
Ameeleza hayo akimjibu Mbunge wa Viti Maalum, Rose Tweve, aliyehoji kuhusu mkakati wa Serikali kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo vya Binadamu kama Figo na Moyo kwa ajili ya wenye uhitaji.
Katika swali la nyongeza Tweve alihoji ni lini Serikali itakuja na muswada wa kuruhusu biashara ya kuvuna viungo ili kuwanusuru Watanzania wanaopoteza maisha kwa kukosa viungo.
“Je Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo kama figo na moyo kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo,” amehoji Tweve.
“Kwa kuwa huduma zimeanza kutolewa, kwa sasa nchi inatumia miongozo ya kimataifa kusimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo,” amesema Mollel.
Aidha, Molel ameeleza kuwa hadi Aprili 2021 hospitali ya Benjamin Mkapa na ile ya Taifa Muhimbili (MNH) zimeshapandikiza figo kwa watu 80 ambapo Muhimbili wamepandikiza figo 62 na Benjamin Mkapa figo 18.