Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemevu, Patrobas Katambi amesema Serikali imeboresha mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya vijana na kupata Mwongozo mpya wa mwaka 2022.
Katambi ameyasema hayo katika kongamano la Vijana Tanzania lililoanza Agusti 3, 2023 Jijini Dodoma na kudai kuwa miongoni mwa mambo yaliyoboreshwa ni fursa ya kijana mmoja mmoja kuweza kukopa, ongezeko la kiwango cha kukopa kutoka Milioni 10 hadi kufikia Milioni 50.
Amesema, “na muda wa mikopo umeongezwa kutoka miezi 24 hadi 36 ambapo asilimia 5 itatozwa kama gharama ya uendeshaji kwa miaka yote mitatu na siyo kila mwaka.”
Katambi ameongeza kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupita Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unalenga kutoa mikopo nafuu kwa vijana ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali, umeweza kutoa mikopo ya Shilingi 1.88 bilioni kwa miradi ya vijana na mwaka huu wa fedha imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi 1.3 Bilioni imetolewa.
“Hivyo, jumla ya mikopo iliyotolewa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/23 hadi Agosti 2023/24 ina thamani ya Shilingi 3.2 bilioni kwa miradi 149 yenye vijana 978 iliyo katika sekta ya Kilimo, Viwanda, Usafirishaji, Biashara na Huduma,” amesema Katambi.
Hata hivyo, amesema katika kuhakikisha kuwa vijana wenye ulemavu wanajengewa uwezo jumla ya vijana wenye ulemavu 407 wamedahiliwa katika vyuo Vitano vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu.