Kaya Zaidi ya 18,103 zenye wakazi wapatao 90,517 Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera zinatarajia kunufaika na upanuzi wa mtandao wa maji kutokana na ujenzi wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa kwa thamani ya shilingi bilioni 2.4 hadi kukamilika kwake.
Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo imetolewa na mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Bukoba (BUWASA) John Sirati juni 24,mwaka huu wakati wa uzinduzi wa vilula vya kuchotea maji uliofanywa na mkuu wa wilaya Bukoba Deodatus Kinawiro katika mtaa wa Kisindi Kata ya Kashai Manispaa ya Bukoba.
Sirati amesema kuwa mradi huo ulianza utekelezaji wake novemba 01,2017 na ulitakiwa kukamilika April 30,2018 lakini kutokana na changamoto mbalimbali mkandarasi alishindwa kukamilisha mradi huo na kuomba kuongezewa muda hadi Desemba 30,2019 ili kukamilisha kazi zilizobaki.
“Kwasasa mradi umekamilika kwa asilimia 95% anachokifanya ni kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizoonekana zina mapungufu chini ya muda wa matazamio ambao utaisha Juni 30 mwaka huu, hata hivyo mradi huu umelenga kuwahudumia wakazi wa kata za Kibeta,Kahororo, Ijuganyondo, Kagondo, Nshambya, Hamugembe,Kashai na baadhi ya maeneo ya kata ya Nyanga.” Amesema Sirati.
Sirati ameongeza kuwa asilimia 96 ya maeneo yote yanayonufaika na mradi huu yameshaanza kupata maji na kuongeza kuwa pindi mradi huu utakapokamilika unatarajia kuongeza eneo la mtandao toka asilimia 88% za sasa hadi asilimia 95% huku mamlaka ikitarajia kuongeza wateja toka 12,284 wa sasa hadi 14,784.
Kwaupande wake mkuu wa wilaya hiyo baada ya kuzindua vilula hivyo ameongea na wananchi waliohudhuria hafla hiyo na kusema kuwa kutokana na kuwepo na tatizo la maji katika manispaa hiyo, serikali ilitoa fedha shilingi billion 32 kwaajili ya mradi mkubwa wa maji kwa manispaa yote ya Bukoba.
Kinawiro amesema anawashukuru BUWASA kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wananchi wa Kisindi kwa kuwajengea Vilula vya kuchotea maji ili kutatua tatizo la maji katika mtaa huo.
Ameongeza kuwa BUWASA bado inaendelea kujenga vilula hivi katika maeneo mengine ili kuhakikisha wananchi wa manispaa wanapata maji na maeneo jirani na kuongeza kuwa serikali inatarajia kutoa fedha nyingine shilingi bilioni 2.5 kwaajili ya kusambaza maji maeneo yote.
Juliet Shangali ni afisa mahusiano wa mamlaka hiyo ameeleza kuwa wananchi watakuwa wakichota maji kwa gharama ya shilingi hamsini 50 kwa kila ndoo moja ya lita 20 huku wakiwauzia maji hayo shilingi 1500/= kwa unit moja ambapo bei hiyo ni chini Zaidi ya watumiaji wengine.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wananchi wa mtaa wa kisindi wameishukuru serikali pamoja na BUWASA Kwa kuwajengea Vilula hivyo vitakavyowasaidia kupata huduma ya maji kwa karibu tofauti na walivyokuwa wakiyafata maji kwa umbali Zaidi ya kilomita 2.
Wananchi hao walisema kuwa walikuwa wakinunua maji kwa shilingi 500 hadi 600 kwa ndoo ya lita 20 suala lililokuwa likiwafanya kutumia fedha nyingi kwaajili ya maji tu ambapo wamesema kuwa mtu mmoja alikuwa akitumia Zaidi ya shilingi elfu 5000 kwa siku kwaajili ya kununua maji, lakini kwasasa shilingi 500 inaweza kutumika kuchota maji ndoo 10.
Mradi huo wa upanuzi wa mtandao wa maji ndani ya manispaa ya Bukoba unatekelezwa na mkandarasi MBESSO Construction Co.Ltd VS COSMOS Engineering Co.Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 2,416,884,958.40 huku fedha ambayo imekwishalipwa ni shilingi bilioni 1,678,904,673.00 utekelezaji wake ukiwa asilimia 95%.