Jeshi la Polisi nchini Haiti limewaua watu wanne na kuwakamata wengine wawili kwa tuhuma za kumuua Rais wa nchi hiyo, Jovenel Moise katika makazi yake.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Leon Charles amewaambia waandishi wa habari kuwa jeshi hilo halitapumzika hadi litakapowakamata au kuwaua wote walioshiriki kufanya mauaji hayo.
“Tulifunga njia zote za kutokea kabla hawajaondoka kwenye eneo la tukio. Kuanzia wakati huo tumekuwa tukipambana nao. Wataua au watakamatwa wote,” alisema Charles.
Jana majira ya saa saba usiku, watu wenye silaha nzito walivamia makazi ya Rais Moise yaliyo kwenye milima ya eneo la Port-au-Prince na kumuua kiongozi huyo. Watu hao walimjeruhi vibaya mkewe, Martine Moise.
Balozi wa Haiti nchini Marekani, Bocchit Edmond amefanya mahojiano na Reuters na kueleza kuwa watu hao wenye silaha nzito waliingia katika makazi ya Rais wakiwa wamevalia sare za maafisa wa Kitengo Maalum cha Marekani cha Kupambana na Madawa ya Kulevya (DEA). Utambulisho wao huo ndio uliowasaidia kuruhusiwa kuingia katika makazi hayo.
Moise aliyefariki akiwa na umri wa miaka 53, aliingia madarakani mwaka 2017. Ameuawa Jumatano wiki hii wakati ambapo nchi yake inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa, wananchi wakifanya maandamano kupinga utawala wake.