Naibu Waziri Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha amesema kuwa Serikali imeshughulikia malalamiko ya wakulima wa Korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa muhimu katika zao hilo.

Ameyasema hayo mapema hii leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge,

Amesema kuwa Serikali imefuta ushuru wa shilingi 20 kwa kilo kwa ajili ya Chama Kikuu cha Ushirika, Shilingi 50 za usafirishaji wa Korosho, Shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya mtunza ghala na pia shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya kikosi kazi cha Masoko.

Aidha, ameongeza kuwa Sekta ina utaratibu maalum wa kupanga bei na dira kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa pamoja na wadau wote.

“Serikali imekwisha fanyia marekebisho maeneo ambayo wakulima walikuwa wanalalamikia kwa kuondoa kabisa makato hayo katika zao hilo”, Amesema Ole Nasha.

Kwa upande wa manunuzi ya pembejeo za korosho amesema hufanywa kwa pamoja na vyombo rasmi ndani ya Tasnia ambapo awali ilikuwa ikisimamiwa na mfuko wa Maendeleo ya Korosho na sasa Bodi ya korosho Tanzania.

Hata hivyo, amezitaja changamoto zinazojitokeza katika kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima wa korosho na hatua zimechukuliwa kwa kushirikisha vyama vya ushirika ili kudhibiti mianya ya pembejeo kwenda kwa wasio lengwa.

Pia Serikali imeweka mfumo wa usambazaji wa pembejeo wenye lengo la kuhakikisha kwamba pembejeo hizo zinawafikia walengwa pekee.

Kampuni ya Highland Estates yapewa siku 30 kusafisha mifereji
Wizara ya Afya kuingia ubia utoaji huduma za uchunguzi wa magonjwa