Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Chiwenga amesema wanakusudia kuanzisha sheria itakayoyafanya mataifa ya nje kutowaajiri wafanyakazi wake wa afya, ikilenga kuzuia upungufu wa wataalamu wa sekta hiyo, huku ikisemekana zaidi ya wauguzi na madaktari 4,000 wameondoka tangu Februari 2021.
Chiwenga, ambaye pia ni Waziri wa afya, amesema kuwa kupoteza kwa wataalamu wa afya ni sawa na ulanguzi wa binadamu na kutangaza adhabu kali zaidi kwa wale ambao alidai wanalinyima taifa mtaji wake wa kibinadamu.
Amesema, “ikiwa mtu ataajiri kimakusudi na kuifanya nchi iteseke, huo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Watu wanakufa hospitalini kwa sababu hakuna wauguzi na madaktari. Hilo lazima lichukuliwe kwa uzito na tutalisimamia vilivyo kwani Zimbabwe inachukia uhalifu huu unaokiuka haki za binadamu.”
Mwezi uliopita (Machi – 2023), Uingereza ilisitisha kuajiri wafanyakazi wa afya wa Zimbabwe baada ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kuwekwa na Shirika la Afya Duniani kwenye orodha nyekundu, ambayo inaashiria nchi zinazokabiliwa na changamoto kubwa za wafanyakazi wa afya.