Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba imemkabidhi Mkandarasi Ms Kajuna Investment eneo la mradi uliokuwa umesimama kwa mda mrefu wa uendelezaji wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi Bukoba, unaotarajia kutumia shilingi 1 bilioni za awali kati ya 18 zinazohitajika, zilizotolewa na Serikali.
Akizungumza na wananchi katika eneo la ujenzi wa kituo hicho cha mabasi Kyakairabwa, Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Manispaa, Steven Byabato amesema uendelezaji wa kituo hicho utasaidia kuepukana na adha ambayo wasafiri wamekuwa wakiipata.
Naibu Waziri wa Nishati, Steven Byabato akizungumza wakati wa mchanganuo wa awamu za fedha za ujenzi wa stendi ya mabasi Kyakairabwa.
Amesema, fedha za ujenzi wa kituo hicho cha mabasi kyakairabwa unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 18 na fedha hizo zitakuja kulingana na awamu za ujenzi hadi kukamilika kwake.
“Tunavyoendelea kuchakata na mambo yalipofikia tutaleta pesa ambazo zitaongezeka katika ujenzi wa stendi, kwahiyo hii awamu ya kwanza ya ujenzi ya bilioni moja isitupe shida, mradi mzima unatakiwa kuwa na bilioni 18 tutarejea tuone hizo gharama na uhalisia wake na pesa zote tunazohitaji,” amesema Waziri huyo.
Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Philbert Gosbert akitoa ufafanuzi wa bilioni moja itakavyotumika ujenzi wa stendi Kyakairabwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara viwanda Biashara na uwekezaji, Philbert Gosbert ametoa ufafanuzi wa fedha hizo zitakavyotumika ikiwemo ujenzi wa eneo la maegesho ya mabasi 26 kwa wakati mmoja, ujenzi wa mabanda tisa ya kusubiria abiria uwekaji wa taa za mionzi ya jua na ujenzi wa mitaro.
Baadhi ya Wananchi walioshuhudia makabidhiano ya ujenzi wa stendi- Kyakairabwa.