Serikali ya Tanzania imefungua rasmi anga la Dar es Salaam na kuruhusu ndege kuingia na kutoka katika jiji hilo, baada ya kuonekana kuwa maambukizi ya virusi vya corona yanapungua.
Waziri wa Miundombinu, Usafirishaji na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi huo ulioanza jana, Mei 18, 2020 ulitokana na kujiridhisha kwa jinsi ambavyo kuna udhibiti dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Alisema kuwa Serikali imefanya utafiti wa kina juu ya hali ilivyo nchini na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo.
Ndege zilizoruhusiwa ni za biashara, diplomasia, za misaada, za dharura na zenye kazi maalum.
Aprili mwaka huu, Serikali ilitangaza kusitisha usafiri wa ndege katika viwanja vyake kutoka nje ya nchi, ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
“Kwa taarifa hii, ndege zote za kimataifa zinaruhusiwa kuingia na kutoka nchini kwetu kuanzia leo,” alisema Mhandisi Kamwele.
Alisisitiza kuwa pamoja na uamuzi huo, Serikali inaendelea kuzingatia muongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya.
Wiki iliyopita, Rais John Magufuli alitangaza kuwa ataruhusu ndege za watalii wanaotaka kuja nchini kufanya utalii na kwamba wataingia bila masharti ya kukaa karantini kwa siku 14.