Serikali kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT) imefuta ada mpya za uendeshaji wa mbio ndefu zinazofanyika nchini baada ya kufanyiwa mabadiliko mwezi Oktoba mwaka jana.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa baraza hilo, Mohamed Kiganja, ambaye amesema uamuzi huo umefanyika baada ya waandaaji wa mbio hizo kulalamika kuwa ada wanayotakiwa kulipa hivi sasa wanailipa mara mbili ikilinganishwa na iliyokuwa ikilipwa mwanzoni.
Baada ya malalamiko hayo, serikali imeagiza waandaji wa mbio ndefu kuendelea kutumia ada za zamani katika uandaaji wa mbio hizo.
Katika hatua nyingine Kiganja amewataka waandaji wa mbio ndefu kuhakikisha wanajisajili ili kuepuka migogoro inayojitokeza mara kwa mara kwenye mchezo wa riadha.