Serikali imefuta miliki ya Mashamba matatu ya Mkomazi Plantantions maarufu MOA yaliyopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya uendelezaji ikiwemo kutelekezwa bila kufanyiwa maendelezo yaliyokusudiwa na kutolipiwa kodi ya pango la ardhi.

Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 30 Agosti 2019 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipozungumza na wananchi wa Mayomboni wilayani Mkinga mkoani Tanga alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.

Mashamba yaliyofutiwa ni lenye hati Na 9780 na ukubwa wa ekari 14,688, shamba Na 4268  ekari 804 na Shamba lenye Hati Na 9781  ekari 246 ambapo mashamba yote matatu yana ukubwa wa ekari 15,738.

Kufuatia uamuzi huo, jumla ya vijiji kumi vyenye kaya 3,236 zilizo na wakazi 16,450 zitanufaika na uamuzi wa serikali kutokana na wananchi wake kuvamia mashamba hayo na kufanya maendelezo ya kujenga makazi, shule pamoja na kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya kudumu na ya muda mfupi.

Aidha, vijiji vilivyonufaika ni uamuzi wa Serikali kufuta mashamba ya Mkomazi Plantations ni kijiji cha Kilulu-Dunga, Zingibari, Mwaboza, Mwakikoya, Mhandakini, Nkanyeni, Sigaya, Mayomboni, Ndumbani pamona na kijiji cha Moa.

Akizungumza wakati wa kutangaza uamuzi huo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema kuwa uamuzi wa kufuta mashamba hayo matatu unafuatia maombi yaliyotumwa kwa Rais John Pombe Magufuli ya kutaka kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa muda mrefu.

Lukuvi ameagiza kufanyika upimaji katika vijiji vyote kumi vilivyopo ndani ya shamba hilo sambamba na kuainishwa mipaka ya vijiji hivyo na kupatiwa hati ambapo alitaka wananchi wanaoishi kwenye vijiji hivyo kutobughudhiwa.

Pia Waziri Lukuvi alitaka maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya uwekezaji katika mashamba yaliyofutwa kuachwa kwa ajili ya shughuli hiyo ikiwemo mwekezaji wa Katani Azka International Tanzania mwenye ekari mia tano pamoja na maeneo ya viwanda kama kile cha kuzalisha chumvi na kusisitiza kuwa serikali inataka uwekezaji utakaotoa ajira kwa vijana na wakati huo kupata mapato kupitia kodi ya pango la ardhi.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa mashamba mengine ya Kwa Mtili Estates Co Ltd yaliyopo Mkinga mkoani Tanga ambapo ekari 58 pekee ndizo zilizoombwa kufutwa kwa Rais kutokana na kutoendelezwa huku mmiliki wake ikidaiwa kumiliki ekari  2,841.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mkinga mkoani Tanga, Dustan Kitandula ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wanaoishi eneo la shamba lililofutwa na kutaka kurejeshewa ardhi yao waliyokuwa wakiitumia kwa shughuli mbalimbali.

 

Viongozi wa CCM wapigwa marufuku kutoa vitisho
Japan yaonya kuhusu madeni ya nchi za Kiafrika