Serikali nchini, imesema itaendelea kuhamasisha upandaji wa mikoko katika maeneo ya pwani kwa ajili ya biashara ya kaboni na kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt.
Selemani Jafo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge yatokanayo na Uchambuzi wa Sheria Ndogo jijini Dodoma.
Amesema kuwa ni kweli maeneo ya pwani yanapata changamoto ya kuliwa na maji ya bahari kutokana na kina kuongezeka hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kujenga kuta na matuta kwa ajili ya kupunguza kasi ya mawimbi ya bahari.
Jafo ameongeza kuwa, Serikali inawakaribisha wawekezaji kutumia fursa hiyo kwa kupanda mikoko katika maeneo ya pwani yenye changamoto za kimazingira kwani baadhi ya maeneo mikoko huchukuliwa na maji hivyo inasababisha kingo za bahari kumomonyoka na maji kuingia nchi kavu na kusababisha mafuruko.