Wakati Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikizidi kuwezesha kazi za wasanii kuwafikia kirahisi na kwa haraka zaidi wadau wa sekta hiyo, Serikali imewataka wananchi kuanzisha utamaduni wa kununua kazi za wasanii hata mtandaoni, kwani ndiyo njia inayoweza kuwanufaisha kwa kazi wanazozifanya.

Wito huo umetolewa wiki hii na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa tovuti a Afro Premiere, iliyoanzishwa kwa lengo la kuuza video za muziki za wasanii.

Alisema mpango huo unaweza kuwa ni moja ya mikakati muhimu ya kupambana na wezi wa kazi za wasanii, kwakuwa video za muziki zitakuwa zikipatikana kwenye mtandao huo peke yake kwa kipindi maalum na hivyo kuingiza pesa zinazoenda kwa msanii, serikali na watayarishaji moja kwa moja.

Aidha, Profesa Gabriel alidai kuwa kwakuwa Afro Premiere itakuwa ikiweka nyimbo za Kiswahili zaidi, itasaidia kukikuza zaidi Kiswahili, ambacho ni cha 10 kati ya lugha elfu sita duniani na kuahidi kupitia wizara ya mambo ya nje, wizara yake itawaunganisha na Watanzania waliopo nje ya nchi.

Msomi huyo aliwataka wasanii wao wenyewe kuunga mkono mpango huo sababu ndio njia pekee ya kuufanya ufanikiwe.

“Mpango huu utafanikiwa kama ninyi mkiwa sehemu ya mpango huu, kama ninyi wenyewe tena mkianza kuwa na kona kona na kuupiga vita, basi mpango huu utaonekana feki na utashindikana,” alisema.

Hadi sasa kuna video mbili mpya zilizowekwa kwenye Afro Premiere ambazo ni Go Low ya G-Nako na Jux pamoja na K wa Roma na Baghdad. Mashabiki wanaweza kununua nyimbo hizo kwa shilingi 300 tu kwa kutumia simu zao.

Kuiona video ya Go Low, bofya link hii>>> http://afropremiere.com/prevideo/1487839158_afropremiere.

Hussein Machozi kurejea na kishindo cha ‘Nipe Sikuachi’ na Man Water
Roberto Mancini Atawala King Power Stadium