Kutokana na ukweli kuwa Wanawake na Vijana ni msingi na chachu ya mabadiliko wa masuala yote ya kiuchumi na kijamii, Serikali imetaka wadau kushirikiana ili kuwezesha makundi hayo kuchangamkia fursa zinazoambatana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Aidha, imesisitizwa kuwa kundi hilo lenye nafasi ya kipekee katika kuelimisha umma juu ya teknolojia mpya za kidijitali, matumizi salama na yenye tija ya TEHAMA, ili kuwesha uchumi wa kidijitali ulio shirikishi kuwa ni lazima liandaliwe kuwa na kasi ya matumizi ya Teknolojia za kidijitali.
Kauli hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele akifungua Mkutano wa wanawake kwenye Kongamano la Saba la Tehama Tanzania, lililoandaliwa na Tume ya Tehama chini ya uongozi wa Dkt. Nkundwe Mwasaga.
Amesema, “Serikali, kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inapenda kuwashukuru wadau wote wa maendeleo ya TEHAMA katika kulitambua kundi hili muhimu na kuendelea kuwezesha wanawake na vijana kuchangamkia fursa zinazoambatana na TEHAMA.“
Kakele ameongeza kuwa, Serikali imeweka mazingira rafiki ya kukuza na kuibua ubunifu, kuchochea uwekezaji na uendelezaji wa Teknolojia za kisasa na TEHEMA kwa kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo mbalimbali.