Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amezihimiza Kamati za maafa nchini kuendelea kuweka mikakati Madhubuti katika kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Ummy ameyasema hayo Mkoani Lindi alipokuwa akifungua kikao kazi cha kujenga uwezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa Mkoani humo kuhusu hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa kilichoratibiwa na Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kimelenga kuifikia Mikoa katika kuzijengea uwezo kamati hizo katika ngazi zote.
Amesema, “Kikao kazi cha leo kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.”
Aidha, Ummy piq alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wajibu wa kila mmoja katika eneo lake la kazi kuendelea kuchukua hatua stahiki endapo maafa yanatokea huku akieleza kuwa mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi yenye jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali za jamii yetu kutokana na matukio ya maafa.
“Uzoefu unaonesha kuwa kuchukua hatua za mapema za kuzuia na kupunguza madhara zimekuwa na gharama nafuu kuliko kusubiri ili kuchukua hatua baada ya maafa kutokea ambapo, serikali imekuwa ikilazimika kutumia fedha nyingi, hivyo tuendelee kujipanga mapema,” alisema Naibu Waziri huyo.