Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametangaza uamuzi wa Serikali wa kuondoa tozo 42 kati ya 47 ambazo walikuwa wanatozwa wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kagera hadi kufikia tozo 5 tu ambazo itakuwa ni jumla ya Shilingi 267 kwa kila kilo ya kahawa, kutoka Shilingi 830 za awali.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maamuzi hayo kufuatia tume maalum aliyoiunda ili kupitia utaratibu na mfumo wa uendeshaji wa vyama vya Ushirika wa zao la kahawa Mkoani Kagera, Hali kadhalika amewaagiza viongozi wa vyama vya Ushirika, wasimamie vyama vyao kwa uaminifu na weledi ili vilete tija kwa wakulima na kuacha tabia ya kukopa pesa benki kwa ajili ya kununua kahawa kwa wakulima.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maagizo hayo Wakati wa Mkutano Maalum wa Wadau wa zao la kahawa mkoani Kagera uliofanyika wilayani Karagwe Mkoa wa Kagera.
Naye Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa kugawa miche ya kutosha ya kahawa kwa wakulima ili ilete tija na kuwaongezea kipato.
Amesema ili kuhakikisha maafisa ugani wanatekeleza majukumu yao ipasavyo Wizara imeandaa utaratibu wa kutoa usafiri pamoja na vifaa vya kupimia udongo
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema kutokana na usimamizi mzuri wa Serikali ya awamu ya sita katika zao la Kahawa, tayari wakulima wemeanza kuona manufaa kwani bei ya zao hilo imepanda.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Tume Maalumu ya kuchunguza mwenendo wa zao hilo. Dkt. Fabian Magawa Madele, alisema katika uchunguzi waligundua ubadhirifu wa zaidi ya shilingi bilioni saba ambazo zilitumika nje ya utaratibu wa vyama vya Ushirika.