Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipongeza timu ya soka ya taifa ya wanawake, “Twiga Stars’ kwa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2024) zitakazofanyika nchini Morocco.

Twiga Stars imeungana na mataifa mengine 12 baada ya ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya Togo juzi Jumanne (Desemba 05) na kuandika historia ya kufuzu kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2010.

Kwa niaba ya Serikali Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, DK Damas Ndumbaro ameipongeza Twiga Stars kwa kuweka ujumbe katika ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii Instagram.

Ndumbaro ameandika: “Ninaipongeza timu ya Taifa ya Wanawake ya mpira wa miguu Twiga Stars’ kwa kufuzu fainali ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON 2024) baada ya ushindi wa jumla wa goli 3-2 dhidi ya Togo. Hongereni sana,”

“Kubwa zaidi niwapongeze wachezaji wetu walitulia na kuzuia mashambulizi mengi hatari na kufanikiwa kuwasukuma katika sehemu ambayo si rahisi kufunga na kupindua matokeo,” amesema Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shimne akizungumzia mchezo huo.

Amesema waliwadhibiti wapinzani wao kuanzia katikati ya uwanja mpaka mstari wa mwisho na kusema kuwa dakika 90 za mchezo huo zilikuwa na ushindani mkali.

“Kipindi cha kwanza tulipoteza nafasi nyingi, washambuliaji wetu walikosa umakini wa kuzitumia na kipindi cha pili tulishambuliwa zaidi kwani wapinzani walikuwa wanalazimisha kucheza,” ameongeza

Mataifa mengine yaliyofuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ‘WAFCON 2024’ ni bingwa mtetezi Afrika Kusini, Botswana, Algeria, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tunisia, Senegal, Zambia, Mali, Nigeria na wenyeji Morocco.

TET yapokea vifaa uimarishaji, utunzaji data
TANESCO waonywa ubebaji changamoto za Wakandarasi