Tume ya Utumishi wa Umma nchini, imetakiwa kusimamia haki wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma yanayowasilishwa, ili kutolewa maamuzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama ameyasema hayo jijini Dodoma, katika kikao kazi na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, kilichofanyika ofisini kwake kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Amesema, Tume ya Utumishi wa Ummainatakiwa kutoa maamuzi ya mashauri yote ya kinidhamu kwa kuzingatia haki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo ili kuweza kuweka usawa baina ya mashauri yanayotolewa.
Waziri amesema, “Tume isipo yashughulikia mashauri ya kinidhamu kwa haki na wakati, inakwamisha maendeleo ya nchi yasipatikane kwa wakati na ndio maana Serikali imekuwa ikiihimiza Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao kwa wakati na kwa kutenda haki.”
“Jambo la msingi hakikisheni haki inatendeka katika mashauri ya kinidhamu, mkifanya hivyo mtakuwa mnasimamia na kujenga nidhamu nzuri ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma,” amefafanua Waziri Mhagama.
Hata hivyo, Waziri huyo pia amezungumzia changamoto za ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma, unaofanywa na baadhi ya waajiri na watumishi na hivyo kuwataka Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma kufanyia kazi suala hilo.
Awali akizungumza mbele ya Waziri Mhagama, Balozi John Haule ameahidi kuwa watatoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma, na kumshukuru kwa kuwahimiza kutenda haki wakati wa kushughulikia mashauri ya kinidhamu.
Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Utumishi wa umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.