Mawaziri sekta zinazotekeleza Mpango wa lishe wamekutana katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kujadili na kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Mwaka wa Wadau wa Lishe utakaofanyika Mkoani Tanga.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mkutano huo kwa kushirikiana na Wizara zinazotekeleza mpango wa lishe pamoja na wadau wa lishe (Joint Multisectoral Nutrition Review) kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe pamoja na mikakati ya Serikali katika kupunguza changamoto ya utapiamlo nchini.
“Suala la lishe ni mtambuka linalosimamiwa kwa ujumla wet una mkitizama sekta ambazo zipo hapa zinaguswa moja kwa moja kwenye suala hili la lishe bora na kupambana na udumavu, utapiamlo na mambo mengine yanayohusu lishe,” Amesema Waziri Mhagama.
Amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kufanikisha hayo imekamilisha maandalizi ya Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Pili wa Masuala ya Lishe (2020/21-2025/26) ambao utatoa mwongozo wa utekelezaji wa afua za lishe hapa nchini kwa miaka mitano.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa, Mkutano huo wa mwaka utafanyika Mkoani Tanga kwa lengo la kuhamasisha wananchi wa Mkoa huo kuongeza jitihada katika masuala ya lishe na hivyo kurudisha mkoa huo katika nafasi iliyokuwa awali na ikiwezekana kufanya vizuri zaidi.