Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili na mauaji ya Wazee, kwa kuongeza msukumo na kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019-2022/2023).

Ameyasema hayo leo Juni 15, 2021 Jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee yenye kauli mbiu “Tupaze Sauti Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee.”

Mwanaidi amesema kuwa kutokana na vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee pamoja na changamoto nyingine zinazoambatana na uzee ikiwemo hofu na wasiwasi, msongo wa mawazo, sonona, upweke, unyanyapaa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, serikali imeweka msisitizo zaidi katika kuhakikisha wazee wanapata huduma ya msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha ili kusaidia kuimarisha afya na ustawi wao.

“Kwa mujibu wa mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisaikolojia wa Mwaka 2021, matatizo mengi ya kiafya na kimahusiano yanayowakabili wazee yanatibika kikamilifu kupitia msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Ameongeza kuwa katika kumlinda Mzee kupitia mpango wa serikali wa kuboresha huduma za afya, serikali imeendelea kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya cha serikali na hospitali zinakuwa na madirisha maalum kwa ajili ya matibabu kwa wazee, ambapo mpaka sasa kuna jumla ya madirisha 2,335 mahususi kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu kwa wazee.

Sambamba na hayo, serikali imeanzisha utaratibu wa kuwa na timu za uratibu katika vituo vya kutolea huduma za afya ambazo zinajumuisha Daktari, Afisa Ustawi wa Jamii na Muuguzi.

Aidha amewakumbusha wananchi wote kwa ujumla kuendelea kutimiza wajibu wa kuwalinda wazee dhidi ya vitendo viovu vinavyohatarisha maisha na uhai wao.

Mwanafunzi wa kidato cha 3 amuua baba yake kwa kipigo kisa ‘kuku’
Mavunde: Tunawatesa watanzania kwa riba kubwa