Katika kukabiliana na athari za ukame, Serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara nchini.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi  Dkt. Charles Tizeba ameyasema hayo leo Mjini, Dodoma katika Kikao  cha Bunge alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula na lishe kwa mwaka 2016/2017.

“Tathimini imebainisha kuwa Halmashauri za wilaya 55 zinahitaji jumla ya tani 1,969 za mbegu bora za mahindi, mtama na mizizi inayokomaa kwa muda mfupi na kustahimili ukame,” amesema Dkt. Tizeba.

Tizeba amezitaja hatua ambazo Serikali inazichukua kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara kuwa ni pamoja na;

Kusimamia usambazaji wa mbegu za mazao ya kilimo zinazostahimili ukame na zinazozaa kwa muda mfupi ambazo ni pamoja na mtama, uwele na mbegu za mazao aina ya mizizi za mihogo na viazi vitamu ili kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha sasa.

Kuhamasisha wakulima kupanda mazao aina ya mizizi, mtama na uwele kwa maeneo yanayopata mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha na mawakala wa pembejeo pamoja na vivutio vya utafiti vilivyopo katika kanda mbalimbali hapa nchini.

Hata hivyo amesema kuwa, hatua nyingine ni Kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula katika maeneo yaliyo na ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Aidha wafanyabiashara waliohifadhi mahindi amewanaomba kusambaza chakula hicho katika masoko ya ndani ya nchi ili kupunguza mfumuko wa bei.

 

Video: Manispaa ya Ilala kuondoa mabango yasiyolipiwa
Makalla atoa siku 14 kwa Halmashauri zote za Jiji la Mbeya