Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari Maelezo imejipanga kupinga ukatili wa kijinsia ndani na nje ya vyumba vya vyombo vya habari kwa kuhakikisha kuwa Tasnia ya Habari inakuwa na sauti moja katika kutetea na kuwawezesha wanawake kwenye vyombo vya habari.

Hayo yamesemwa katika mkutano wa kupanga mradi wa kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari katika kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto na wadau mbalimbali wa kupigania haki za waandishi wa habari wanawake unaoendelea mkoani Morogoro.

Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Habari Mkuu na Mwakilishi kutoka Idara ya Habari Maelezo, Ingiahedi Mduma alipokuwa akielezea nafasi ya Wizara katika kukabiliana na ukatili wa ndani na nje ya chumba cha habari, amesema kuwa Serikali kupitia Idara hiyo imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ya unyanyasaji wa kijinsia wanaofanyiwa wanawake ndani na nje ya chumba cha habari na kuweka wazi mikakati mbalimbali ya Wizara ambayo itawezesha kukabiliana na tatizo hilo.

Mduma amesema kuwa, Serikali imejipanga kukomesha ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vya habari kwa kutoa ushauri na kuwatambua waandishi wa habari wanawake kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini na kujitambua ili waweze kukabiliana na waajiri wao na kuepukana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

“Kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi ya wasimamizi/ wahariri wanatabia ya kuwalaghai wasichana ili wafanye nao mapenzi kwa kuwadanganya kuwa watawaajiri. Tabia hii inaenda kinyume na maadili ya taaluma ya uandishi wa Habari, hatua thabiti zitachukuliwa pale itakapobainika na kuthibitika kuwa kumetendeka unyanyasaji wa kijinsia ndani na Nje ya vyumba vya habari,” amesema Mduma.

Aidha ameongeza kuwa Serikali Inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya habari ili kuwawezesha waandishi kutekeleza majukumu yao bila hofu, na kwa kujiamini huku wakizingatia sheria, kanuni, maadili na weledi ili wananchi waweze kupata habari sahihi kwa ajili ya manufaa ya Taifa na maendeleo yao.

Mkutano huo umekuja kufuatia maazimio ya Mkutano wa siku ya uhuru wa vyombo vya Habari Duniani ambao kitaifa ulifanyika Jijini Arusha Mei 3,2021.

Mtibwa U20 waula Morogoro
Mingange: Simba itawapigeni sana 4, 4