Serikali imedhamiria kutumia jukwaa wa Mashindano ya AFCON U17 yatakayofanyika hivi karibuni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kunufaika na wageni mbalimbali watakao kuja kushiriki michuano hiyo ya Kimataifa.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda wakati wa kikao na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa lengo la kuhakiki mikakati itakayotumika kutangaza vivutio hivyo ambavyo ni tunu ya Taifa.

“Sisi Wizara ya Maliasili na Utalii tutahakikisha tunatumia jukwaa hili la michezo kuongeza idadi ya watalii katika vivutio vya utalii nchini na tumejipanga vizuri kwa matangazo mbalimbali ambayo yanamvuto wa ushawishi kwa watalii hawa wa michezo kuvutiwa kufika katika maeneo hayo tunafukwe nzuri, Mbuga za wanyama, Majengo ya kale yenye hishoria mbalimbali, Maporomoko ya maji na Mlima Kilimanjaro,”amesema Prof. Mkenda.

Aidha, amesisitiza kuwa ujio wa mashindano hayo ya AFCON U17 nchini ni jambo lenye manufaa makubwa kwa taifa kwani kwa kujipanga vizuri huu ndio wakati wa kunufaika kwa watanzania wote kupitia wageni hao, wajasiriamali mbalimbali watanufaika kwa namna moja kwani wageni hao watahitaji huduma mbalimbali kwa kipindi chote watakapo kuwa hapa nchini hivyo ni vyema watanzania watumie fursa hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Susan Mlawi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo kwani fedha hizo zitasaidia kukamilisha uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika kipindi cha mashindano.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wilfred Kidao amesema kuwa katika mashindano hayo Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani, Gianni Infantino atakuja hivyo ujio wake katika mashindano hayo utakuwa ni fursa ya kutangaza nchi yetu, vilevile uongozi wote wa shirikisho la mpira wa Miguu Afrika (CAF) nao utahamia Tanzania katika kipindi chote cha mashindano.

 

Rais wa Algeria atangaza tarehe ya kujiuzulu
Serikali yawaonya waliojipanga kuhujumu miradi