Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amefanya ziara ya kukagua ufikishaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika bandari ya Mtwara uliofanywa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), upatikanaji wa mawasiliano
ya simu katika eneo hilo pamoja na mifumo ya TEHAMA inayotumika bandarini hapo.
Katika ziara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo ameambatana na wataalam kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo ambazo ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) pamoja na wenyeji wake ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini Mhe. Dunstan Kyobya na wabunge wa majimbo
matatu yaliyopo katika Mkoa wa Mtwara ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Mtwara ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, \
Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, mwingiliano wa mawasiliano mipakani na usikivu wa radio ya Taifa TBC.
“Nimefika hapa kujiridhisha uwepo wa nyaya za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika bandari ya Mtwara zitakazofanikisha upatikanaji wa intaneti yenye uwezo mkubwa na kasi kubwa ili shughuli zote zinazoendelea bandarini zisikwame kwasababu ya kukosekana kwa
huduma ya intaneti” alizungumza Mhandisi Kundo.
Aidha, pamoja na kukagua ufikishaji wa miundombinu ya Mkongo wa Taifa katika bandari hiyo pia alitumia muda huo kukagua mifumo ya TEHAMA inayotumika kwenye bandari hiyo kama inafanya kazi na kusomana na kutoruhusu mianya ya upotevu wa mapato na kukagua upatikanaji wa mawasiliano ya simu katika eneo la bandari hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Mhandisi Kundo alizungumzia mwingiliano wa mawasiliano ya simu na nchi jirani ya Msumbiji yaliyolalamikiwa na wabunge na kutolea ufafanuzi kuwa mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani yanasababishwa na uwezo wa minara ya mawasiliano iliyopo eneo husika pamoja na ramani ya mipaka ya kijiografia ya eneo husika inavyoingia na kutoka hivyo kusababisha eneo lenye mtandao wenye nguvu zaidi ndio utakaopatikana.
Aliongeza kuwa Wizara hiyo ipo katika hatua za kuhakikisha minara inayojengwa kuanzia sasa inakuwa na uwezo wa 3G na kuendelea pamoja na kuiboresha minara ya zamani iliyokuwa na uwezo wa 2G kwenda 3G na kuendelea ili kuhakikisha kunakuwa na mitandao yenye nguvu itakayowezesha kupatikana kwa huduma ya mawasiliano ya simu na intaneti.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge wa majimbo matatu ya Mtwara Mjini Mhe. Abdallah Chikota (Mb) Nanyamba, Mhe. Hassan Mtenga (Mb) Mtwara Mjini na Mhe. Issa Mchungaela (Mb) Lulindi, mbali na kuzungumzia mahitaji ya huduma za mawasiliano katika maeneo yao kwa niaba ya wananchi pia walitumia fursa hiyo kumshukuru Mhandisi Kundo
kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana ili kutatua changamoto za mawasiliano zilizopo katika Mkoa huo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari