Naibu katibu mkuu ofisi ya Rais tawala za mikoa na Serikali za mitaa Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wafamasia nchini kupambana na wabadhilifu wa dawa zinazotolewa na serikali kwenye vituo vya huduma za afya na kutafsiri falsafa ya hapa kazi tu kwa vitendo.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo katika kikao kazi cha wataalau hao kinachofanyika Jijini Dodoma na kudai ni lazima kuipambania sekta ya afya ambayo ni muhimu na ndio maana katika mwaka wa fedha 2019/2020 serikali imepitisha bajeti ya Shilingi bilioni 57.4.
“Ni lazima kupambana na wabadhilifu wa dawa maana sekta ya afya ni muhimu na lazima tuitafsiri falsafa ya hapa kazi tu kwa vitendo maana Rais Magufuli anafanya kazi kubwa na ndio maana bajeti ya shilingi bilioni 57.4 imetengwa na katika vipaumbele vitatu vya pesa hizo na dawa ni kimojawapo” amefafanua Dkt. Gwajima.
Amesema pamoja na mapambano dhidi ya wabadhilifu pia wataalamu hao wanatakiwa kutumia mfumo wa ugavi dawa ambao kimsingi taarifa zake huingizwa na kutumika kuombea dawa ambapo mfamasia wa Mkoa atakuwa na wajibu wa kuhalalisha maombi husika kwenda bohari ya dawa (MSD).
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa katika zoezi hilo mikoa itakayoanza ni pamoja na Singida, Dodoma, Manyara, Kagera na Geita na kwamba taarifa ya kila mkoa itawasilishwa ofisi ya Rais TAMISEMI kwa lengo la kuchakata taarifa za mifumo ya dawa ili kubaini kama kuna dawa za kutosha.
“Kwa mfumo huo wa medical audit utasaidia kupata taarifa mbalimbali ikiwemo kujua kama kuna hifadhi ya dawa ya kutosha au la na wataalamu wetu watatusaidia katika hilo ili taarifa zinazofika ofisi ya Rais TAMISEMI iweze kuzifanyia kazi,” ameongeza Gwajima.
kali ipo katika maboresho ya mfumo wa uendeshaji wa shughuli za afya ambao ukikamilika utatoa taarifa za makusanyo ya fedha za dawa hadi ngazi ya mtumiaji wa mwisho.
Awali Mkurugenzi wa idara ya afya na ustawi wa jamii ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema sekta ya afya imekuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Rais Magufuli hivyo wataalamu wanatakiwa kuonesha kwa vitendo kuwa Rais hajakosea katika machaguo yake na vipaumbele alivyojiwekea katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku kwa Taifa.
“Mhe. Rais alielekeza katika ziara zake kuwa sekta hii ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo nchi hasa wakati huu tunapoelekea katika uchumi wa kati ifikapo 2025 na toka ameingia madarakani ameendelea kutenga fedha kwaajili ya kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya,” amefafanua Dkt. Kapologwe.
Amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 vituo vya afya 352 zikiwepo Hospitali 9, Vituo vya Afya 304 na Zahanati 39 zilikarabatiwa huku vituo vinavyo jengwa na kukarabatiwa vikiwa vimefikia 470 zikiwemo hospitali 67 mpya za Halmashauri ambazo zitakuwa na idara kamili ya dawa.
Kikao cha wafamasia kimetayarishwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuziba mianya ya ubadhilifu wa dawa na kuweka mikakati endelevu ya upatikanaji wake sehemu za kutolea huduma za afya.