Serikali ya Nigeria imekiri kuwa kambi ya jeshi la ulinzi ilivamiwa na magaidi wa Boko Haram katika jimbo la Borno, Kusini Mashariki mwa nchi hiyo.
Imeripotiwa kuwa takribani wanajeshi 40 waliuawa katika shambulizi hilo lilitekelezwa Jumapili iliyopita, baada ya wapiganaji wa Boko Haram kuvamia kambi ya jeshi ya Matele.
Ikiwa imebaki miezi mitatu tu nchi hiyo ifanye uchaguzi mkuu, Serikali imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuna hali ya utulivu.
Rais Muhammadu Buhari, ambaye anagombea nafasi ya kuchaguliwa kwa awamu ya pili, aliahidi kulitokomeza kundi la Boko Haram alipokuwa anawania Urais mwaka 2015. Kundi hilo la kigaidi linapambana na Serikali kwa lengo la kufanya mapinduzi na kusimika utawala unaofuata sheria za Kiislamu.
Ingawa jeshi la Nigeria limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti maeneo ambayo awali yalikuwa yanashikiliwa na Boko Haram, kundi hilo bado limeendelea kufanya mashambulizi ya kushtukiza yanayochukua uhai wa watu wasio na hatia.
Hata hivyo, idadi ya wanajeshi wanaouawa kwenye mashambulizi ya Boko Haram bado yanazua utata, kwani Serikali imekuwa ikieleza kuwa idadi kubwa inayotolewa si ya kweli na kwamba inasaidia kuhamasisha uwepo wa kundi hilo.
Boko Haram ililoanzishwa mwaka 2002 katika eneo la Maiguduri nchini Nigeria; ni mshirika wa kundi la kigaidi la Islamic State (IS). Mwaka 2015, lilitangaza kubadili jina na kuitwa Islamic State in West Africa na hivi sasa linafanya shughuli zake za kigaidi katika maeneo ya Kaskazini mwa Cameroon, Chad na Nigeria.