Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kujenga mustakabali wa nchi yetu.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Juni 26, 2022 katika ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mteule Wolfgang Pisa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi katika viwanja vya Ilulu, Lindi.
“Maendeleo ya nchi hayawezi kuimarika kama tutakuwa wabinafsi. Tukiimarisha ushirikiano na ushirikishwaji wa kila mtu, tutaleta maendeleo ya Taifa letu kwa haraka,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali imeendelea kushirikiana na dini zote katika kukuza ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii ili kuimarisha maisha ya kila Mtanzania na Taifa kwa ujumla.
Majaliwa amesema miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kuwaongoza watu kiroho kwa kuwapa mafundisho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani.
“Vilevile, mmekuwa mkiwasaidia watu katika shida mbalimbali hususan wale wenye uhitaji kama yatima na wajane sambamba na kutoa ushauri nasaha na malezi bora kwa vijana.”