Serikali imesema, inaandaa mkakati utakaosaidia nchi kuondokana na tatizo la ujangili ifikapo mwaka 2025, kupitia utekelezaji wa mradi jumuishi wa kupambana na tatizo hilo na biashara haramu ya Wanyamapori .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa tatu wa Kamati tendaji ya mradi huo hii leo Juni 27, 2022 uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dodoma.
Amesema, lengo la mkutano huo ni kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi na kutoa mwongozo kwa Kitengo cha Usimamizi kuhakikisha kinafanya kazi kikamilifu ili kufikia lengo la Serikali la kutokomeza suala la ujangili na kupambana na biashara haramu za wanyamapori.
“Wizara ya Maliasili na Utalii inasimamia ushirikiano kati ya washirika na wadau katika utekelezaji wa mradi ili kufikia dira ya sera ya Taifa ya Wanyamapori inayolenga kulinda wanyamapori na makazi yao na maendeleo ya rasilimali za wanyamapori,” amefafanua Prof. Sedoyeka.
Aidha, amesema mradi unalenga kupambana na ujangili kupitia kanuni za uwindaji wa Kitalii, kuwajengea uwezo watumishi katika kupambana na ujangili, kuwawezesha wananchi kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu na kushiriki katika usimamizi wa wanyamapori.
Mkutano huo, umehudhuriwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo Duniani (UNDP), Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji wa Mradi na Kitengo cha Usimamizi wa Mradi.