Serikali kupitia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, imelaani kitendo cha kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi Jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF).
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas imesema kuwa wamechukua muda kidogo kulifuatilia suala hilo na kubaini kuwa wengine waliharibiwa vifaa vyao licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi.
“Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii,”amesema Dkt. Abbas
Aidha,Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kina ainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.
Ameongeza kuwa Misingi ya uhuru wa kitaaluma imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi imeuridhia.
Hata hivyo, amesema kuwa kwa kuwa suala hilo tayari limeripotiwa polisi, amewaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe