Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amelifungia gazeti la Mseto   kwa miezi 36 kutokana na kuchapisha habari za uongo na kugushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali.
Uamuzi huo wa kulifungia gazeti la Mseto  umetolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 242 lilitolewa tarehe 10Agosti 2016 kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 Sura ya 229,Kifungu 25(1).
Mhe. Nape Moses Nnauye ameeleza kuwa Kifungu hicho kinampa mamlaka yeye kama Waziri kuchukua uamuzi wa kufungia Gazeti kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari za uongo na kugushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali.
“Serikali kwa masikitiko makubwa imelazimika kilifungia gazeti la Mseto  kutokana na mwenendo wa uandishi wa kuandika na kuchapisha habari za uongo na kugushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais  wetu wa Awamu ya Tano  Mhe.Dkt.John Pombe Mgufuli na viongozi wa Serikali” Alisema Mhe Waziri Nape.
Aidha Mhe. Nape amesema kuwa hatua ya kulifungia gazeti la Mseto imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda  mrefu kuanzia Septemba,2012 hadi Agosti,2016 kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kuacha kuandika  habari za upotoshaji,uchochezi na za uongo na zisizo zingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa Habari bila mafanikio.
Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayoanisha Uhuru wa Habari na mipaka ya habari kama vile tamko la Haki za Binaadamu la mwaka 1948 ambapo nchi yetu imeruhusu kwa kiwango kikubwa  kwa kuweka ukomo wa uhuru huo kwa kukataza habari za uzushi uongo na uchochezi.
Gazeti la Mseto limezuiwa kuchapishwa katika njia nyingine yeyote ikiwemo mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya  Kieletroniki na Posta Sura ya 306

Wizara Ya Afya Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Upungufu Wa Chanjo Homa Ya Manjano
Naibu Waziri Mpina Atembelea Taasisi Za Muungano Kwa Upande Wa Zanzibar