Serikali imeitaka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS), kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi ili kuhakikisha kuwa inatetea maslahi ya Wananchi na Taifa.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro ameyabainisha hayo wakati wa kikao kazi na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, iliyoongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Nalija Luhende kilichofanyika jijini Dar es Salaam kujadili utekelezaji wa majukumu.
Amesema, ni muhimu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaiwakilisha vema Serikali na taasisi zake kwenye mashauri ya madai na usuluhishi ili kuhakikisha inalinda hadhi ya Serikali na wananchi wake.
“Wizara hii imeshikilia haki ya wananchi, amani na utulivu wa nchi na uwekezaji, hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata haki yao kwa mujibu wa katiba na sheria
za nchi zilizopo, tuzingatie suala la amani na utulivu katika kuvutia uwekezaji,” amefafanua Dkt. Ndumbaro.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Ofisi hiyo kwa niaba ya Menejimenti, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende amesema tangu kuanzishwa kwa Ofisi hiyo mwaka wameendesha mashauri 5,905 ambapo kati ya hayo 5,768 ni ya madai na137 ni ya usuluhishi.
Dkt. Luhende ameongeza kuwa, “ili kufikia azma ya kupanua wigo wa utendaji wa Ofisi na kuongeza ukaribu katika kuhudumia wananchi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ina Ofisi 17 ambazo zimefunguliwa kwenye mikoa yote yenye masjala za Mahakama Kuu ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.”
Ameitaja Mikoa mingine kuwa ni Dodoma, Mtwara, Iringa, Ruvuma, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Mara, Mwanza, Kagera, Shinyanga,Tabora, Rukwa, Mbeya na Morogoro.
Dkt. Ndumbaro, yupo jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi na atazungumza na taasisi za Wizara hiyo ikiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Tume ya Haki za Binadamu, Wakala wa Vizazi na Vifo, na Taasisi ya Msaada wa Kisheria ili kujadili utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.