Serikali imenunua magari 12 ya wagonjwa pamoja na kliniki mbili zinazotembea (mobile clinics) kwa ajili ya kuwasaidia majeruhi wa ajali kabla ya kufikishwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa uamuzi huo wa Serikali unatokana na ukweli kuwa majeruhi wengi wa ajali hupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitalini kwa kukosa huduma ya awali.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndugulile, magari hayo yameshawasili nchini na yataanza kufanya kazi wakati wa mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika – (SADC), baada ya hapo yatasambazwa kwenye mikoa yenye uhitaji.

“Baada ya mkutano wa SADC tutasambaza katika mikoa mbalimbali na tutahakikisha kuna vituo maalum vinavyotoa huduma ya afya baada ya watu kupata ajali mbalimbali,” amesema Dkt. Ndugulile.

Amefafanua kuwa huo ni mfumo ulioanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha inaokoa maisha ya Watanzania ambao wanapoteza maisha saa chache baada ya kupata ajali barabarani kutokana na kukosa huduma ya haraka ya matibabu ya awali.

Aidha, Dkt. Ndugulile ameeleza kuwa Serikai iko kwenye mchakato wa kununua vifaa vya uokoaji katika majanga ya moto. Amesema vifaa hivyo ni pamoja na magari ya uokoaji.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa anaamini huduma ya magari ya wagonjwa pamoja na mafunzo yatakayotolewa yatasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi.

Watu takribani 76 walipoteza maisha kutokana na ajali ya moto uliozuka baada ya gari la mafuta kuanguka katika eneo la Msamvu Mjini Morogoro, Agosti 10, 2019. Kati yao, waliofariki baada ya kufikishwa hospitalini au wakiwa njiani wakikimbizwa hospitalini ni zaidi ya 15.

*Picha kwenye habari sio gari lililonunuliwa na Serikali

Je, bado unatafuta ajira? hizi hapa nafasi za kazi kutoka makampuni 8 Tanzania
Majeruhi wengine wa ajali ya moto Morogoro wafariki dunia