Shirika la Reli nchini, TRC leo limenunua vichwa kumi na moja vya treni kwa bei ya dola Milioni Nane na Laki Nane ili kuliongezea ufanisi wa kazi shirika hilo.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu was TRC, Msanja Kadogosa imesema kwa sasa TRC ina vichwa 29 madhubuti kati ya 47 vinavyovihitajika ili kutoa huduma bora zaidi.
Vichwa hivyo 11 viliingizwa nchini katika bandari ya Dar es Salaam Julai 2017 na kampuni ya Progress Rail Locomotives ya Marekani, PRL, kwa ajili ya kuviuza.
Kwa kuhitaji vichwa hivyo serikali iliunda timu ya wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, TEMESA na TRC kwa ajili ya kubaini kama vichwa hivyo ni vipya au la.
Baada ya uchunguzi na ukaguzi wa vichwa hivyo, kamati ilibaini kuwa ni vipya na hivyo serikali kuamua kutiliana saini na kampuni ya PRL ili kuvinunua.
Hata hivyo ili kujihakikishia zaidi ubora wake, vichwa hivyo vitafanyiwa majaribio katika awamu tatu, ikiwemo kuvitazama kwa nje, kuviwasha na kuvipa mzigo vikiwa havitembei na tatu ni kuvifunga kuvuta mabewa vikiwa na mzigo wa tani 700 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kuviongezea mzigo wa tani 1,200 kutoka Morogoro hadi Kigoma na Mwanza.
TRC imetiliana saini leo jijini Dar es Salaam na kuvinunua vichwa hivyo, huku TRC ikihakikishiwa ubora wa vichwa hivyo kwa garanti ya miaka miwili.