Mawakili wa Serikali katika kesi inayowakabili viongozi saba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ameiomba Mahakama kusikiliza kesi hiyo kwa siku mfululizo ili kuharakisha uamuzi wake.
Akiwasilisha ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Wilbard Mashauri, Wakili wa Serikali , Faraja Nchimbi alieleza mahakama kuwa kesi hiyo inapaswa kwenda haraka kutokana na ukweli kuwa watuhumiwa wengi ni wabunge wanaopaswa kuhudhuria vikao vya Bunge vilivyoanza.
Pia, Wakili Nchimbi aliongeza kuwa ushahidi wa kesi hiyo umekwishakamilika na kwamba kesi hiyo inavuta hisia za watu wengi.
Hata hivyo, Wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala alipinga ombi hilo akiieleza mahakama kuwa yeye kama wakili kiongozi wa upande huo atakuwa na kesi nyingine katika Mahakama Kuu pamoja na kutakiwa kuhudhuria kikao cha Chama Cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) jijini Arusha.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri alikubaliana na hoja ya Kibatala na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16 mwaka huu.
- Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Aprili 4, 2018
- Bocco aigalagaza Njombe Mji FC, atumbukiza mawili
Mbowe na viongozi wengine sita waandamizi wa chama hicho walipewa dhamana jana baada ya kushikiliwa kwa takribani siku saba mahabusu wakikabiliwa na kesi ya uchochezi na kufanya maandamano bila kibali.
Akizungumza baada ya kutoka mahakamani, Mbowe alisema kuwa ameyaona mengi alipokuwa mahabusu na kwamba atayaweka wazi.
Wengine waliounganishwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji, Manaibu wakuu wa Bara na Visiwani, John Mnyika na Salumu Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mhazini wa Baraza la Wanawake, Esther Matiko.