Mamlaka nchini Afrika Kusini imetoa onyo kwa migahawa kutumia mbinu mbalimbali kuuza pombe na kukiuka marufuku ambayo imeweka hivi karibuni kufuatia ongezeko la maambukizi ya Covid 19.
Waziri wa Polisi, Bheki Cele, amesema migahawa itakayokiuka agizo itanyang’anywa leseni na wamiliki kufunguliwa mashtaka.
Cele ameionya migahawa hiyo na kuitaka kutoweka pombe kwenye chupa za chai au zile zilizoandikwa hakuna kilevi akisisitiza wanafahamu mbinu hizo zote.
Awali, Rais Cyril Ramaphosa alisema vitendo vinavyotokana na unywaji pombe vimechochea hatari ya mlipuko kuendelea kusambaa katika nchi hiyo ambayo hivi karibuni imeripoti aina mpya ya Kirusi cha Corona.
Afrika Kusini ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya Virusi vya Corona na hivi karibuni ilirejesha baadhi ya vizuizi kutokana na hali kuwa mbaya tena.
Hadi sasa tayari Afrika Kusini imeripoti visa zaidi ya Milioni moja ambapo kati ya hao zaidi ya watu 850,000 wamepona na wengine zaidi ya 27,000 wamefariki dunia.