Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa amewonya wafanyabiashara wanaopandosha bei za bidhaa sokoni na maduka ya ujenzi hali inayowafanya wa wananchi wahitaji wa bidhaa hizo kuzikosa kutokana na gharama.

Majaliwa ameyasema hayo leo Alhamisi Februari 10, 2022 wakati akijibu swali la Mbunge wa Msalala (CCM), Iddi Kassim kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo amehoji nini kauli ya serikali kuhusiana na mfumko wa bei za vyakula ikiwemo mafuta, sabuni na vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na majibu.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Majaliwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika akiongeza kuwa upandaji wakati mwingine ni wa makusudi unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua kali na kusimamia upandaji wa bei hizi zisiendelee kupanda wakati wote. Naagiza Taasisi yetu ya FCC kusimamia haki za wafanyabiashara katika kufanya biashara, ihakikishe inafanya ukaguzi wa kina kwa bidhaa zinazozalishwa na mauzo yao walinganishe na uzalishaji wao kwa mwaka,” aliongeza Majaliwa.

Pia amesema upandaji huo wakati mwingine husababishwa na upandaji wa malighafi lakini viwanda vingi vya nchini vimekuwa vikitegemea malighafi zinazozalishwa nchini ambazo zipo.

Majaliwa amesema wafanyabiashara wamekuwa wakiwekeana mikataba na Serikali na pia wakati wanajenga mazingira wezeshi ya biashara nchini, jambo kubwa lilikuwa ni kupata bidhaa kwa wingi, kwa bei nafuu na kuwezesha kupatikana wakati wote lakini wafanyabiashara wengine wameanza kukiuka hayo.

Amesema siku si nyingi Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji aliliambia Taifa upo mkakati unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wa kupandisha bei kwa makusudi.

Amesema miongoni mwa makusudi hayo ni wazalishaji kuzalisha bidhaa kidogo na hivyo kutengeneza upungufu mtaani ili bei zipande na kumekuwa na utamaduni wa uovu wa wafanyabiashara wa kukaa kwa pamoja na hivyo kusababisha bei za bidhaa kupanda.

“Ndio maana Waziri (Dk Kijaji) ametoka hadharani kutueleza mkakati wa Serikali. Naunga mkono mkakati huo lakini natoa agizo kwa wafanyabiashara kuacha tabia hiyo ovu inayopelelea jamii kushindwa kupata bidhaa kwa gharama nafuu,” amesema Majaliwa.

Amesema lengo ni kufahamu kama wanazalisha kwa kiwango kile kile walichokubaliana ama wamepunguza uzalishaji ili kutengeneza upungufu na pia kama bidhaa zimepanda wafahamu kwanini wamepandisha bei.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la bei za bidhaa tofauti na waziri Mkuu ameliahidi Bunge kuwa Serikali italifanyia kazi kupitia taasisi zake kama ilivyoelezwa na Waziri Dk Kijaji.

Siku ya wapendanao kuwa chungu kwa aliyempiga mkewe mjamzito
Sera ya habari kupitiwa upya