Katika kuwawezesha Wanawake kiuchumi, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi 600 milioni, huku ikilenga kuendelea kuwahamasisha kujiunga na majukwaa mbalimbali ya ufanikishaji wa mpango huo kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata, Halmashauri, Mkoa na Ngazi ya Taifa
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima hii leo Julai 30, 2022 wakati akiongea na vyombo vya Habari majukumu ya Wizara na utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema, Serikali itaendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, ikiwemo kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
“Mwanamke ndiyo mlezi wa familia hivyo anahitaji kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na taendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, tutaratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi yao,” amesema Waziri Gwajima.
Ameongeza kuwa, katika kuimarisha majukwaa hayo Wizara itasambaza mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi pamoja na kuzindua mpango huo Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa lengo la kufikia matarajio kusudiwa.
Kuhusu mipango juu ya makundi maalum, Gwajima amesema Wizara imetenga Shilingi 45 Bilioni kwa kundi wafanyabishara wadogo maarufu kama wamachinga kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya masoko na kuwawezesha kupata mitaji ya kuendeleza biashara mbalimbali wanazozifanya nchini.
Aidha, Dkt. Gwajima pia amesema kwa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wizara imetenga kiasi cha Shilingi 5.3 Bilioni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii nchini.
Utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, OR-TAMISEMI, Fedha na Mipango, Mambo ya Ndani ya Nchi, Uwekezaji, Viwanda na Biashara, OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.